Nimeamua
kuandika makala hii kuhusu sekta ya Elimu na Uchumi wetu, hii ni kutokana hali
ya mabadiliko ya maisha ya hapa Tanzania kwa kupanda gharama za maisha na hata
kuongezeka kwa ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa fani mbalimbali. Mfano, tunapozungumzia
mabadiriko ya kiuchumi pamoja na ukuaji wa utandawazi kote duniani, hii ikiwa ni
kutokana na kuwepo kwa viashiria vya mabadiriko yanayotokana na presha ya ukuaji
wa kasi katika sekta mbalimbali kote duniani, hasa kiteknolojia, uchumi na hata
hali ya masoko ya fedha (ambapo shilingi inazidi kushuka) na bidhaa mbalimbali,
pamoja na huduma za kijamii na kibiashara zitolewazo ndani na nje ya nchi.
Kwa
kiasi kikubwa Tanzania inaathiriwa na nchi ambazo ziko mbele kiuchumi, uchumi
huo hasa nautizamia katika sekta kuu tatu (3), ambazo ni sekta ya kilimo,
viwanda, na hata sekta ya huduma za kijamii na kibiashara. Kwa mapana yake ni
kwamba sekta hizo ndizo ambazo zinajenga uchumi wa nchi na kuhakikisha unakua
kadiri ya mipango endelevu kulingana na vipaumbele vya taifa husika.
Nikirudi
kwenye sekta ya Elimu, kama nilipotaja hapo juu ya kuwa yafaa nchi yetu iwe na
mfumo wa Elimu kwa mgawanyiko wa miaka 8+2+2+2+3. Ikiwa na maana ya mgawanyiko
wa madaraja matatu (3) ya Elimu. Ukianza na miaka 8 kwa Elimu ya Msingi, kisha
miaka sita (6) yani (2+2+2) kwa Elimu ya Sekondari na miaka mitatu (3) kwa Elimu
ya Chuo Kikuu. Kwa mtiririko wa madaraja haya matatu naendelea kuyaelezea hapa
chini kama ifuatayo;-
Daraja
la kwanza ni la Elimu ya Msingi (Primary Education) kwa miaka 8. Ambapo miaka
saba (7) itakuwa ni ya huduma ya taaluma kama jinsi ilivyo sasa, isipokuwa
wanafunzi wanaofikia darasa la nne (4) na kupasi mitihani yao itawapasa waanze
kujifunza fani maalumu hadi wanapomaliza darasa la saba (7), na wanapofikia mwaka
wao wa mwisho, ikimaanisha darasa la nane (8) wataingia katika mafunzo maalumu
kwa vitendo. Hivyo, huu unakuwa ni mwaka wa kuingia karakana za kujifunza fani
mbalimbali za ufundi stadi, kilimo na sayansi za jamii. Katika ufundi stadi
kuna fani mbalimbali kama ufundi uashi, uchomeleaji vyuma, umeme, uselemara,
makenika, na hata fani nyinginezo kama kompyuta, udeleva, kilimo na ufugaji,
ushonaji, ufumaji na hata sanaa mbalimbali. Mafunzo mengineyo ni kama ya kazi
za ndani, afya, usafi, mapishi na lishe, biashara, pia mafunzo ya hoteli na utalii,
maarifa ya nyumbani, ususi wa mitindo ya nywele nayo yanaweza kuanzia katika
daraja hili. Hivyo, huu unakuwa ni mwaka wa kumuandaa kijana ili aweze
kupambana na hali ya maisha kwa namna ya kijasiriamali, ili pindi amalizapo Elimu
yake ya Msingi aweze kuingia katika soko la ajira na kuweza kukuza na kuongeza
uwezo wa uzalishaji mali na kipato cha familia. Pia mwaka wa 8 waweza
kutambulika kama mwaka wa Elementary & Foundation Courses. Kufuzu vizuri
kwa daraja hili pia kutaweza kumuandaa muhitimu kuweza kujiunga na Elimu ya
Sekondari (Secondary Education).
Daraja
la pili ni la Elimu ya Sekondari (Secondary Education) kwa miaka 6. Ambapo daraja
hili lina mgawanyiko wa Elimu ya Sekondari ya Kawaida (Ordinary Level) kwa
miaka 4 yani (2+2) na Sekondari ya Juu (Advanced Level) kwa miaka 2. Hivyo
Elimu ya Sekondari ya Kawaida ni miaka 4, iliyogawanyika kwa awamu 2 tofauti
yani (2+2). Maana yake ni kwamba mika 2 ya mwanzo itakuwa ni ya mafunzo ya
nadharia kutokana ya Elimu ya Msingi aliyojifunza mwanafunzi mpaka darasa la 8.
Miaka 2 mingine itakuwa ni ya nadharia na vitendo zaidi. Awamu hii ya pili
itaweza kumjengea mwanafunzi uwezo mkubwa zaidi ya ule alioupata wakati wa
mafunzo ya darasa la 8. Mfano kama darasa la 8 alijifunza ufundi umeme kwa
uwezo wa ngazi ya Elementary & Foundation Courses, basi mwanafunzi huyu atakapofikia
hatua hii ya Elimu ya Sekondari atajifunza kiundani zaidi fani ya umeme kwa
ngazi ya cheti cha Elimu ya Sekondari ya Kawaida (Certificate of Secondary
Education Examination) ambayo itakuwa ni sawa na kupata Astashahada ya Ufundi
Umeme (Certificate in Electrical Technician) ambayo itakuwa ni sawa na ile
inayotolewa VETA. Kwa maana hiyo muhitimu wa kidato cha nne (4) atakuwa tayari
amemaliza shule ya Sekondari ya Kawaida (Ordinary Level) huku akiwa tayari na
ujuzi wa kutosha kuweza kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe. Japokuwa atakuwa
amebakiza miaka mingine 2 ya Elimu ya Sekondari ya Juu (Advanced Level).
Elimu
ya Sekondari ya Juu (Advanced Level) kwa miaka 2. Hii itakuwa ni Elimu ya
daraja la kati la kumuandaa mwanafunzi kuweza kufuzu vizuri na kujiunga na
Elimu ya Chuo Kikuu. Elimu hii itakuwa inamjenga mwanafunzi kupanda daraja
kulingana na fani anayoisomea na kujipatia ujuzi zaidi kwa ngazi ya cheti cha
Elimu ya Sekondari ya Juu (Advanced Certificate of Secondary Education
Examination) ambayo ni sawa na Stashahada ya Ufundi Umeme (Diploma in
Electrical Technician au (FTC). Kwa maana hiyo muhitimu wa kidato cha sita (6) atakuwa
tayari amemaliza shule ya Sekondari ya Juu (Advanced Level) huku akiwa tayari
na ujuzi wa kutosha kuweza kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe.
Daraja
la tatu ni la Elimu ya Chuo Kikuu (University Education) kwa miaka 3. Hii itakuwa
ni elimu ya juu kwa ngazi ya menejimenti na utawala, pia itakuwa ni ngazi ya
kuwapa fursa wanazuoni kuweza kujikita katika kuendeleza uweledi wa fani na
hata ujuzi walioanza kuwanao tangia wakiwa darasa la 8 la Elimu ya Msingi. Kwa hali
hii pia itaweza kuongeza uzalishaji mali na huduma kwa soko la ndani ya nchi. Kwa
upande mwingine Elimu ya Chuo Kikuu itaweza kukuza, kuboresha na kuongeza fani na
huduma za utafiti na ubunifu katika sekta mbalimbali zinaoweza kupambana na
ushindani wa uzalishaji mali mbalimbali na huduma za kiofisi na bishara ambapo
zitatuletea ukuaji bora na wa uhakika kwa soko la ndani na nje ya nchi yetu. Kwa
maana hiyo yule aliyeanza kujifunza ufundi umeme tangia akiwa Elimu ya Msingi,
anapohitimu mafunzo yake ya Elimu ya Chuo Kikuu atakuwa na Shahada ya Uhandisi wa
Umeme (Bachelor Degree in Electrical Engineering). Kwa maana hii, hata katika mfumo wa ajira, anapokuwepo Engineer mmoja katika kazi atapaswa kuwa na wasaidizi wa nne (4) katika daraja la Stashahada (Diploma au FTC) na pia wasaidizi wengine nane (8) wa daraja la Astashahada au Certificate (Full Task Force = 1 Engineer + 4 Technitians + 8 Artisans). Nadhani kwa kupitia muongozo huu, mpaka hapa utakuwa umeshanielewa kuwa ni jinsi gani tatizo la ajira litakavyo pungua, kutokana na kuwaongezeka wananchi fursa na uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe, na hasa kwa ngazi za madaraja ya chini, hususani kwa wahitimu wa ngazi ya Certificate na Diploma, na hivyo kuongeza nguvukazi ya uzalishaji na ujenzi wa uchumi wetu.
Nimejaribu
kuandika makala hii kutokana na mfumo wetu wa elimu kuwa na mapungufu mengi na makubwa
zaidi, mapungufu hayo nipamoja na kutokuweza kumuandaa muhitimu wa daraja
lolote kuweza kuingia katika soko la ajira au kujiajiri mwenyewe. Mfano, mhitimu
wa Elimu ya Msingi kwa sasa ajira yake kubwa na ya haraka ni kazi za ndani (House
boy/girl) au uchuuzi wa bidhaa ndogondogo na huduma nyinginezo kama vibarua,
vilabu vya pombe, na hata kuingia kwenye huduma za usafirishaji abiria na
mizigo, ambapo kwa asilimia kubwa kazi hizi zimebakia kuwa sio rasmi kwa muda
mrefu sasa. Mfano mwingine ni pale panapotokea kuwapo kwa muhitimu wa Elimu ya
Sekondari, kwa kati ya kidato cha nne au sita (Form 4 & Form 6) imekuwa ni
kwaida kukuta mwanafunzi anapofeli masomo yake analazimika kwenda Mafunzo ya Ualimu,
cha ajabu hapa ni kwamba aliyefeli Elimu ya Sekondari ndiye anayeandaliwa kuwa
mwalimu wa kizazi kijacho, mtu huyohuyo ndiye anayeandaliwa kuwa askari polisi
wa kusimamia haki na usalama wa jamii yetu! Lakini pia ukizingatia yule
aliyepata matokeo mazuri naye hakuandaliwa kujiariri aku kuajiriwa kutokana na
kukosa mafunzo ya fani mbadala inayokidhi soko la ajira na kumfanya aanze
kusomea kozi maalumu nje ya masomo aliyoyasomea katika Elimu ya Sekondari.
Kwa
maana hii, tukifanikiwa kuunganisha elimu yetu ya taaluma ya kawaida na ile
yenye mafunzo ya fani mbalimbali na ufundi stadi, tutaweza kukabiliana na tatizo
la ajira pamoja na matatizo mengineyo yanayo pandisha gharama za maisha kwa kila
mwaka, pia itasaidia kuwezesha sekta binafsi kukua kwa kasi na kuweza kujidhatiti
katika uzalishaji mali na bidhaa za ndani, ambapo pia tutaweza kutumia
rasilimali zetu wenyewe na hatimaye kukuza uchumi wa ndani, kupunguza uingizaji
wa bidhaa za kutoka nje ya nchi kwa kushindanisha na bidhaa zetu wenyewe, na hatimaye
kupunguza umasikini Tanzania. Mjadala huu
unaweza kuendelea kwa kuchangia maoni yako pia!
No comments:
Post a Comment